TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Sunday 8 September 2013

Young Killer: Kipaji kilichogunduliwa na Fiesta super nyota


Young Killer

Eriki Msodoki maarufu kama Young Killer ni msanii mdogo na chipukizi katika tasnia ya muziki wa bongo. Alizaliwa miaka 19 iliyopita jijini Mwanza katika familia ya watoto sita, na yeye akiwa ni mtoto wa mwisho.

 Ni msanii ambaye ana kipaji kikubwa, jinsi anavyoimba muziki wa bongo fleva mtaani hupenda kusema muziki wa kufoka foka au mchano, utafikiri ni msanii ambaye aliwahi kuwepo katika sanaa hiyo kwa muda mrefu kutokana na kuimba kwa kujiamini akiwa stejini.


Kila mwanamuziki ukimuuliza ulianzia wapi kuimba muziki, wengine watakwambia shule na wengine watakwambia wamerithi kipaji pengine kutoka kwa baba, mama, mjomba, dada, kaka na shangazi.

Kwake yeye young killer anakwambia alianza kupenda muziki  wakati huo akiwa anasoma darasa la tatu katika shule ya msingi Lake Mwanza. Anasema alikuwa akipenda kusikiliza na kufuatilia muziki  na hata kuimba kipindi anapokuwa amekaa mwenyewe.

Mbali na kuimba, alikuwa akipenda pia kufuatilia muziki sio tu wa Tanzania hadi wa kimataifa. Msanii ambaye alimvutia  kuingia katika muziki ni msanii wa Marekani Lil Bow na mwingine wa Tanzania ni Fid Q, kwani anavutiwa sana na jinsi wanavyochana mistari.

“Wanamuziki hao nawakubali sana ndio walinifanya leo hii mimi nifanye vizuri, nimekuwa nikiwafuatilia jinsi wanavyoimba, na mimi nimekuwa nikijitahidi kufuata nyendo zao ili niweze kufika mbali kimuziki,”anasema.

Historia ya Lil Bow ya muziki ilikuwa inaonyesha kuwa alianza muziki akiwa na miaka mitatu, na aliendelea kutamba na kufahamika sehemu mbalimbali duniani, na kupata mafanikio makubwa.

Hali kadhalika, Fid Q, ni msanii  mkongwe anayekubalika Tanzania na kimataifa, ambaye ana mafanikio makubwa kimuziki.

Young Killer anasema yeye pia alianza muziki akiwa ni mtoto, alikuwa anasoma lakini pia muziki aliupa nafasi yake  ingawa hakupata nafasi ya kurekodi hadi alipomaliza darasa la saba mwaka 2008.

Msanii huyu anajivunia kuwa licha ya kuwa alikuwa akiimba muziki wakati anasoma  lakini aliweza  kufaulu kwenda Sekondari  ambapo mwaka 2009 alijiunga  na shule ya Sekondari ya Mwanza.

“Nilipofanikiwa kuingia kidato cha kwanza niliendelea na muziki, na hapa niliupa kipaumbele zaidi, kwani nilikuwa najitahidi kutafuta sehemu za kuimba ili kipaji changu kionekane,”anasema.

Anasema alikuwa akichanganya masomo na muziki kwani wakati wa usiku alikuwa akihudhuria klabu mbalimbali za Mwanza na kuomba kuimba jukwaani.
Hakuona shida wala madhara ya kuchanganya muziki na masomo, alikuwa ana ratiba zake, kuna muda wa kusoma na muda mwingine alikuwa akijichanganya klabu.

Anasema alikuwa akipata changamoto kubwa kutafuta shoo kwani wakati alipokuwa akienda katika klabu mbalimbali kwa ajili ya kuomba kuimba, alikataliwa kwa vile alikuwa akionekana bado ni mtoto.

Hata hivyo, alikuwa sio mtu wa kukata tamaa, baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari, alikutana na mtayarishaji wa muziki aliyefahamika kama Duke, ambaye walisaini kufanya kazi pamoja chini ya studio inayoitwa Dar Laboratori.

Chini ya studio hiyo alifanikiwa kurekodi kwa mara ya kwanza wimbo wake unoitwa Tungo ambapo aliimba kwa staili ya kufoka foka,lakini haukufanya vizuri  na hivyo pia hakusikika sana.

Anasema akarekodi tena nyimbo zake nyingine kama tunaumia, winner, matatizo na chambua lakini zote hizo hazikufanikiwa kufanya vizuri.
Msanii huyo anasema hakukata tamaa aliendelea na juhudi za kupambana ili aweze kutoka na kufahamika.

Kwa bahati nzuri, mwaka 2012 kulikuwa na shindano la kusaka vipaji lililokuwa linaitwa Fiesta super nyota ambalo liliandaliwa na kituo cha utangazaji cha Clouds kwa mikoa yote Tanzania, lengo likiwa ni kupata vipaji vitakavyowakilisha katika tamasha la Fiesta.

Anasema walipofika Mwanza alijitokeza akiwa na vijana wengine wengi ili kupata nafasi ya kutangaza kipaji chake. Anasema kila mmoja aliimba, nay eye ndiye aliyekuwa mshindi wa jumla akitokea Mwanza.

“Nilishukuru kwasababu kipaji changu  kilionekana na hatimaye mimi nilichaguliwa kuwa mshindi kwa upande wa Mwanza,”anasema.

Anasema kwa mara ya kwanza aliweza kupata nafasi ya kufanya shoo za fiesta Mwanza, na kufanikiwa kuzunguka mikoa yote ya Tanzania na wasanii wakubwa na kufanya nao shoo mbalimbali.

Kubwa ambalo anasema hatosahau katika maisha yake ya kimuziki, mara baada ya kupata nafasi alipanda jukwaani na kuimba  maiki moja na msanii wa Marekani Riki Rose, kwani hakuwahi kuota kukutana naye wala kupanda jukwaa moja, hilo kwake lilimpa faraja kubwa.

Anasema ni jambo hatolisahau akiamini kwamba Tanzania kuna wasanii wengi wakubwa, lakini hawajawahi kupata nafasi kama hiyo ya kuimba jukwaa moja na msanii huyo, lakini yeye ni msanii mchanga mwenye bahati kubwa.

Wakati anatoka katika mzunguko wa fiesta tayari mkataba wake wa mwanzo ulikuwa unaisha, hivyo akapata tena nafasi ya kujiunga na studio nyingine ambayo yuko nayo hadi sasa inaitwa Classic Sound chini ya mtayarishaji wa muziki Mona Gangstar.

Anasema kupitia mkataba mpya, ndipo alianza kuitambulisha ngoma yake mpya inayoitwa Dear gambe, ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika chati za muziki wa bongo kutokana na mashairi yake kuwagusa watu.

“Nashukuru Mungu wimbo wangu wa dear gambe unazidi kufanya vizuri kwani ndio wimbo ambao unanifanya nipate shoo, kutokana na kukubalika kwa mashabiki wangu,”anasema.

Mbali na wimbo huo, siku za karibuni aliachia tena wimbo mwingine unaoitwa jana na leo aliomshirikisha Stamina na Quick Racka, na bado unaendelea kufanya vizuri.

Na sasa bado anaendelea kuvuma na ngoma yake inayofahamika kama ‘Mrs superstar’.

Young Killer ni msanii mdogo lakini ana akili nyingi, anajivunia kwamba baada ya kupata fedha kutokana na shoo za Fiesta na kupitia muziki wake wa dear Gambe, alinunua mchanga tela mbili na sementi mifuko mitatu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yao ya kifamilia.

Anasema kwa jinsi walivyojipanga katika familia yao, kila mtu alipangiwa anunue kitu chake ili kukamilisha ujenzi wa nyumba yao, nay eye hivyo, ndio vitu ambavyo alipangiwa na familia yake.

Pamoja na hayo, anasema akipata mafanikio makubwa kimuziki atamjengea mama yake nyumba nzuri, kumpa gari ya kutembelea na kutoa mitaji kwa ndugu zake ambao wanaishi katika mazingira magumu ili wafanye biashara itakayowakomboa.



4 comments: